Monday, September 24, 2012

TANZANIA UTALII FESTIVAL YAZINDULIWA!

Bodi ya Utalii Tanzania na Nugaz Event Planner Kufanya Tamasha la Utalii Tarehe 27-28 Oktoba, 2012. Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Aloyce Nzuki (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nugaz  Antonio Nugaz bango la taarifa za tamasha la Utalii linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam mwezi ujao ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa tamasha hilo. Halfa hiyo ilifanyika Dar es Salaam jana ambapo kampuni ya Nugaz ya Dar es Salaam itaandaa tamasha hilo kwa uratibu wa TTB

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Aloyce Nzuki (kushoto) akikafafanua jambo kwa waandishi wa habari hawapo pichani Dar es Salaama jana kuhusu tamasha la Utalii linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam mwezi ujao ikiwa ni jitihada za TTB katika kuutangaza utalii wa ndani.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nugaz  Antonio Nugaz inayoandaa tamasha hilo chini ya uratibu wa TTB.

MAELEZO YA MKURUGENZI MWENDESHAJI WA BODI YA UTALII TANZANIA DR. ALOYCE NZUKI KUHUSU TAMASHA LA UTALII (UTALII FESTIVAL) KWA WAANDISHI WA HABARI 24/09/2012.
Lengo la mkutano huu ni kutambulisha rasmi Tamasha la aina yake hapa nchini.
 
Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Nugaz Event Planner tumeamua kuanzisha tamasha la Utalii linalojulikana kama Tanzania Utalii Festival litakalokuwa linafanyika kila mwaka. Kauli mbiu ya tamasha hii ni “Enjoy Nature Experience Culture”.
Tamasha hili litaanza rasmi mwaka huu ambapo litafanyika tarehe 27-28 Oktoba kijiji cha Makumbusho na litakuwa linaanza saa nne asubuhi hadi saa nne usiku.
Tamasha hili litahusisha shughuli mbalimbali kama vile ngoma za asili za makabila yetu hapa nchini, vyakula na vinywaji vya asili vya makabila mbalimbali, n.k.  Aidha, tamasha hili litahusisha vikundi mbalimbali kutoka katika mikoa yetu ya Tanzania Bara na Visiwani ambavyo vitakuwa vinaalikwa  kushiriki katika tamasha.
Katika tamasha hili kutakuwa pia na usiku wa Utalii.  Huu utakuwa ni usiku maalum kwa wale watakaokuwa wameshindwa kuhudhuria tamasha wakati wa mchana kutokana na sababu mbalimbali.
LENGO LA TAMASHA
Wazo la kuwa na tamasha hili limetokana na hali halisi ya idadi ndogo ya watalii wa ndani yaani watanzania wanaotembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii.  Hivyo Bodi ya Utalii Tanzania na Kampuni ya Nugaz Event Planner tukakubaliana kuwa na tamasha hili kwa lengo la kuhamasisha Utalii Tanzania hususani Utalii wa Ndani, lakini pia tunaamini litasaidia kuongeza mapato ya serikali.
Tunapenda kuwaalika watanzania wote kuhudhuria katika tamasha hili kwa kiingilio kidogo cha Tsh. 2000/=.
Tumeanzisha tovuti mahsusi kwa ajili ya tamasha hili ambayo ni www.tanzaniautaliifestival.com.
Hivyo kwa taarifa zaidi kuhusu tamasha hili tunawaomba mtembelee tovuti hii. 

No comments:

Post a Comment